GIFT KIPAPA

Saturday, July 9, 2016

WHEN I SAY I LOVE YOU BOOK 1



 BY D.G.LWASYE 'GIFT KIPAPA'

Mwanzoni mwa mwaka 2000, mwaka ambao haukuwa mpya peke yake bali pia ulikuwa ni mwanzo wa karne mpya ya ishirini na moja. Watu walikuwa wana tarajia mambo mengi sana mwaka huo ikiwa pamoja na vitisho kama vile mwisho wa dunia na kutokufanya kazi kwa kompyuta, yote hayo yalikuwa ni chachu zilizoufanya mwaka huo uwe wa kipekee.
Katika ofisi ya makao makuu ya dayosisi ya mbeya iliyo chini ya dhehebu la kirutheli, kulikuwa na vijana wengi wa rika moja waliokuwa wamekaa katika mapokezi ya ofisi hiyo iliyopo katika wiliya ya tukuyu.
Vijana hao walikuwa ni wanafunzi wapya wa  shule ya sekondari iitwayo
‘MANOW JUNIOR SEMINARY’
inayomilikiwa na dayosisi hiyo.
Walikuwa hapo wakisubiri basi la shule liwapeleke mahali ilipo shule yao ili wakaanze masomo yao ya sekondari kwa mara ya kwanza.
Japo wengi wao walikuwa hawafahamiani lakini wakajikuta wanazoeana katika kipindi hicho kifupi walichokuwa hapo. Waliongea na kucheka pamoja kwa ujumla wote walikuwa na furaha ya kwenda kujiunga na masomo ya sekondari hasa hasa sekondari ya bweni, kwani kwao yalikuwa ni maisha mapya  waliokuwa wakiyaota pindi walipokuwa shule ya msingi, wakiamini kwamba wakiwa bweni  watakuwa huru na sheria na miiko ya wazazi wao.
Waliongea mambo mengi lakini zaidi ni juu ya maisha ya bweni , kila mmoja aliongea kile alichowahi kusikia kuhusu bweni.
Wengine walisema  wanafunzi wa vidato vya juu wanawatesa na kuwatumikisha wanafunzi wa kidato cha kwanza huku wengine wakisema hayo yalikuwa ni mambo ya kizamani , siku hizi hakuna anyeingilia uhuru wa mwenzake.
“piiii!, piiii!”
Ilisikika honi toka kwenye gari moja la kifahari aina ya hammer lililokuwa likiingiia katika maegesho ya ofisi hiyo.
Wanafunzi watatu wa kike ndio waliokuwa wakipigiwa honi hiyo. Walikuwa wamesimama katika maegesho hayo wakipiga stori mpaka kujisahau. Walisogea pembeni huku wakicheka, waliliangalia gari hilo lililokuwa na vioo vyeusi yenye uwezo wa kumzuia mtu wa nje asione ndani  ya gari.
Matairi ya gari hilo yalisimama mara baada ya kuegeshwa vizuri katika maegesho hayo kisha mlango wa upande wa dereva ulifunguliwa na kisha mtu aliyekuwa akiendesha alishuka.
Sura za wale mabinti waliokuwa wakilikodolea gari hilo zilibadilika ghafla na kujawa na taharuki hata kicheko chao kilikatika, hakuna yoyote kati yao aliyeamini kile alichokiona.
Hii ilikuwa ni kwa mara ya kwanza kwao kumuona mvulana wa rika lao akiendesha gari la kifahari namna hiyo, na haikuwa juu ya gari peke yake bali pia  mavazi yake, cheni pamoja na saa ya mkononi, kila kitu kilikuwa ni ghari ni kama vile walimuona nyota wa muziki hip hop  nchini marekani.
Sekunde chache baada ya kijana huyo kushuka mlango wa upande wa pili ulifunguliwa ambapo alishuka mzee mmoja wa makamo alievalia suti ya rangi ya kahawia. mara baada ya kushuka toka ndani ya gari hilo, mzee huyo aliliangalia jengo la ofisi hiyo kisha akatabasamu, akaanza kupiga hatua kuelekea ulipo mlango wa ofisi hiyo ambapo yule kijana aliyekuwa nae alimfuata.
Wale wasichana watatu waliendelea kumkodolea macho kijana huyo mpaka alipotokomea ndani ya ofisi hizo.
“Mambo ya vibopa hayo!”
aliongea mmoja  kati ya wasichana hao akimaanisha mambo ya matajiri, wenzake hawakuongea jambo lolote zaidi ya kucheka na baada ya muda mfupi waliendelea na maongezi yao waliyokuwa wakiongea mawanzoni na kusahau habari za yule kijana, waliendelea kuongea huku wakicheka na kufurahi.
“Unaona basi nikamwambia huwezi kuju…………”,
msichana huyo alikatiza kile alichokuwa akiwaeleza wenzake na kisha ukimya ulitawala kati yao kwa muda fulani huku wote watatu wakiwa makini na kitu fulani, hii iliwatokea mara baada ya kijana yule aliepita wakati ule, akitoka ndani ya ofisi na kutembea kwa mwendo wa taratibu kuelekea kule alikoegesha gari yao, ukimya uliendelea kuwapo kati ya wasichana hao huku macho yao yakimnyemelea kijana huyo.
Kijana huyo ambaye kwa muonekano hakuwa na sura yenye mvuto wala macho yenye kuvutia sana wasichana, yeye alikuwa wa kawaida sana kiasi cha kuweza hata kudharaulika hata mbele za msichana yeyote yule mwenye kuumbika,  kifupi mvulana huyo alikuwa mbaya wa sura na hata umbo, lakini cha ajabu wasichana hao walionekana kumkodolea macho kupita kiasi mpaka kufikia hatua ya kusitisha maongezi yao.
Mvulana huyo alienda moja kwa moja lilipo gari lao na kuliegamia na kisha kutoa simu iliyokuwepo mfukoni mwake na kupiga namba fulani. Wasichana wale watatu waliacha midomo wazi kwa mshangao baada ya kuiona simu ya mvulana huyo ambayo ilikuwa ni simu ya gharama sana kiasi cha wasichana hao kutowahi kuiona maishani mwao.
“Vipi sister” alianza kuongea kijana huyo mara baada ya simu aliyokuwa akipiga kupokelewa.
“Tumefika salama tu, ila uchovu tu” aliendelea kuongea kijana huyo huku bado wale wasichana wakiendelea kumwangalia,
“Robert Jackson!” aliita mama mmoja aliyekuwa amesimama kwenye mlango wa kuingilia kwenye ofisi hiyo, kauli hiyo ilimfanya kijana yule akate simu hata bila ya kuagana vizuri na aliyekuwa akiongea nae.
“Naam” kijana yule aliitika akiwa amesimama wima.
“Unahitajika kwenye ofisi ya Askofu” aliongea mama huyo mara tu akageuka na kuingia ndani ya ofisi hiyo.
“Kumbe anaitwa Robert Jackson” aliongea mmoja kati ya wale wasichana waliokuwa wakimwangalia kijana kwa sauti ya chinichini,
“Mm! Vicky unampenda nini?”
msichana mwingine alihoji kwa sauti ya chini pia kisha wote watatu walicheka kwa sauti huku wakigonganishaa mikono yao.
Robert alitembea haraka haraka kuelekea kule alikoitwa, hakuwasikia kabisa wasichana hao kile walichokuwa wakiongea na wala hakuhisi kwamba wasichana hao walikuwa wakimzungumzia, mbali na yote hakuwazingatia kabisa, kichwani mwake yeye aliyafikiria mambo yake tu.



“Ndiyo Ndugu Askofu huyu ndio kijana wetu anaitwa Robert”,
“Sawasawa Ndugu Jackson anaonekana ni kijana safi sana, karibu kijana”,
“Asante, shikamoo”,
“Marahaba, keti basi”,
“Asante”
Robert alishukuru na kisha kuketi kama ambavyo alielekezwa, macho yake yote yalimwangalia Askofu huyo akimsikiliza akiongea
“sasa Ndugu Jackson kijana wako amepokelewa, ila nafikri hakupata barua ya maelekezo, ni kwamba simu, mikufu na cheni hatuvihitaji vitu hivyo katika shule yetu, nguo ni zile tu ambazo kijana atavaa atakapokuwa anaenda likizoni hatuhitaji nguo zozote zaidi ya uniform tu”.
“Hilo nafikiri halina tatizo ndugu Askofu”
aliongea Mzee Jackson bila kujua kwamba ni jinsi gani kauli hiyo ilivyo msononesha kijana wake.
Kwa Robert kutokuwa na simu kwa kipindi chote atakachokuwa shuleni itakuwa swala gumu sana kwake kwani simu hiyo ndio kitu pekee alichokuwa akitegemea kitakachoweza kumuunganisha na familia yake kwa wakati atakapo ikumbuka.
Kichwani mwake aliamini kuishi bila simu kutamfanya awe katika mazingira magumu mno.
“Sijui itakuwaje du!”
Aliwaza akiwa bado yumo ndani ya ofisi ya hiyo ya Askofu pamoja na baba yake, baada ya kumaliza mazungumzo hayo na Askofu, Mzee Jackson aliagana na Askofu na kisha wakatoka ndani ya ofisi hiyo wakiwa na mwanae ambapo alitakiwa kumuacha Robert ili aungane na wanafunzi wenzake wanaosubiria usafiri kwa ajili ya kuwapeleka shuleni kwao.
Robert alimsindikiza baba yake mpaka alipopanda gari.  alihuzunika kuona baba yake anaichukua simu pamoja na begi lake alilowekea nguo pamoja na makororkoro yake yote na kurudi nalo.
“Ndio unaniacha baba!” aliongea Robert akiwa kama vile haamini kinachoendelea,
“Ndio mwanangu, najua una wasiwasi, ondoa huo wasiwasi hayo ni maisha ya kawaida tu”
“Lakini nitawakumbuka sana”
“hilo lisikupe shida, lazima ujifunze maisha ya peke yako”
aliongea mzee Jackson kwa kumpa moyo kijana wake.
Robert alitabasamu mara baada ya baba yake kumweleza kauli hiyo lakini macho yake bado yaliendelea kuonyesha huzuni, ilikuwa vigumu kwake kuyazoea maisha hayo katika mazingira mapya kabisa huku hata watu pia ni wapya katika macho yake.
“Baki salama mwanangu nakutakia masomo mema”
aliongea Mzee Jackson akiwa amemkumbatia mwanae.
“Nashukuru baba, na wewe nakutakia safari njema”
mara baada ya maongezi hayo Mzee Jackson aliingia ndani ya gari yake tayari kwa kuanza safari yake. Alipoliwasha tu gari hilo kilichofuata ni kupungiana mikono mpaka alipotokomea kabisa, alikuwa akielekea katika Manispaa ya Mbeya, ambapo alipanga kwenda kupumzika ili mapema siku inayofuata aianze safari ya kurejea jijini Dar es Salaam, ambako anaenda kujumuika na mkewe pamoja na binti yake.
Upande wa Robert huzuni iliongezeka mara mbili zaidi pale aliposhuhudia matairi ya gari la baba yake yakianza kusaga ardhi ya mji wa Tukuyu, alijiona kama kifaranga cha kuku kilichoachwa na mama yake katika pori, kwa unyonge akajivuta mpaka pale mapokezi mahali ambapo wanafunzi wenzake walikaa, akakaa kwenye moja ya viti vilivyokuwepo hapo, huku bado mawazo yakiwa yamejaa kichwani mwake.
Huzuni aliyokuwa nayo ilikuwa kubwa kweli kweli alitamani hata kulia lakini aliona aibu kufanya hivyo mbele ya wanafunzi wenzake, hivyo akaona ni bora aendelee kujikaza tu. Akiangalia pande zote hakuna hata mtu mmoja aliekuwa akimfahamu kati ya waliokuwa ndani ya mapokezi hivyo jambo hilo lilimnyima raha kupita kiasi, alijikuta anajikalia kimya pasipo kumwongelesha mtu yoyote.
Nusu saa baadae basi moja jeupe liliingia katika maegesho ya ofisi hiyo, kwa kusoma maandishi tu Robert aligundua kwamba hilo ndilo basi la shule.
‘MANOW JUNIOR SEMINARY’
Hivyo ndivyo yalivyosomeka maandishi hayo yaliyokuwa  yameandikwa kwenye ubavu wa basi hilo. Mara tu baada ya basi hilo kuegeshwa wanafunzi wote waliambiwa waingie ndani ya basi hilo, Robert alikuwa ni mmoja kati ya wanafunzi walioingia mapema zaidi katika basi hilo, alikaa siti ya saba upande wa kushoto, siti ambayo hukaliwa na watu wawili tu, wakati ile ya upande wa kulia hukaliwa na watu watatu.
“Tuwahi siti ile”
mmoja kati ya wale wasichana watatu alietambulika kwa jina la Vicky alisikika akiongea huku akinyooshea mkono kwenye moja kati ya siti za upande wa kulia ambazo zilikuwa bado kukaliwa na watu, alisema hivyo sababu alitaka wakae siti moja wote watatu ili kuendeleza maongezi yao wakiwa ndani ya basi hilo.
“Ona Vicky nimekwishawahi hivi”
aliongea msichana tena kati ya wasichana hao huku akiwa amekalia mwishoni mwa siti hiyo ili kuzuia mtu mwingine kukaa siti hiyo zaidi ya rafiki zake.
“Safi sana ume………”
Vicky alikatiza kauli hiyo baada ya kuifikia siti hiyo hali hiyo ilimkuta mara baada ya kuangaza macho yake katika siti ya saba upande wa kushoto, alimwona Robert akiwa ameketi peke yake katika siti hiyo ya watu wawili
Akajikuta anaahirisha papo hapo mpango wa kukaa na rafiki zake siti moja na kuwahi haraka kwenye siti aliyokalia Robert kabla mtu mwingine hajakaa kwenye siti hiyo.
“Uuh”
Vicky alishusha pumzi kwa nguvu mara baada ya kufanikisha zoezi hilo la kukaa kwenye siti hiyo, rafiki zake walikwisha gundua kitu kilichomfanya Vicky aende kukaa kwenye siti hiyo wakabaki wanacheka huku wakigonganisha mikono yao.
Pamoja na Vicky kushusha pumzi kwa nguvu kiasi kile Robert hakugeuza kichwa chake kumwangalia Vicky, aliendelea kuangalia dirishani ambako ndiko alikokuwa anaangalia toka alipo ingia ndani ya basi hilo.
Vicky  hakutaka kuiacha hali ya ukimya kati yao iendelee hata kwa dakika moja, akaamua kumwongelesha.
“Mambo”
Vicky alisalimia huku akiwa mametoa tabasamu zito usoni kwake.
Robert aligeuza shingo yake toka huko dirishani alikokuwa akiangalia mara  baada ya kusikia sauti hiyo nyororo ambayo hata kama ingelisikika kwenye ngoma za masikio ya nyoka aliyeko pangoni basi lazima angetoka nje, macho yake yalikutana moja kwa moja na uso wa Vicky uliokuwaumefunikwa na tabasamu zito lililomfanya Robert apumbazike kwa sekunde kadhaa.
“Nakusalimia”.
Vicky aliongea kwa sauti laini na yenye mnato baada ya kuona Robert hajajibu salamu yake. Sauti hiyo ililimzindua Robert na kumfanya ajishtukie kwa vile alivyokuwa  na kuona aibu kuyaangalia macho ya Vicky.
“Ah poa tu”
aliitikia salamu ya Vicky lakini kwa wasiwasi mno na kisha kugeukia upande wa dirishani tena.
“Naitwa Vicky”
aliongea tena akiwa na lengo lile lile la kutoa ukimya kati yao huku akiwa ametabasamu alimwangalia Robert ambae bado alikuwa ameangalia upande wa dirishani, lakini aligeuza sura yake na kumuangalia Vicky mara baada ya kupata utambulisho wa jina kwa Vicky, alipogeuka tu akakutana tena na tabasamu la Vicky na kujikuta nae pia anatabasamu.
“Ah Vicky una jina zuri sana”.
“Asante, na wewe unaitwaje?”
“Robert”
“Oh jina zuri sana”
“Asante”
Robert aliongea huku  macho yake yakimgeukia Vicky, Vicky nae alimuangalia Robert lakini kwa jicho la wizi.
Basi liliendeleza mwendo huku ndani yake zikisikika kelele za wanafunzi waliokuwa wakicheka kwa furaha huku wakiambizana haya na yale.
Maongezi kati ya Robert na Vicky yaliendelea na kuzidi kupamba moto, kwa muda huo mfupi, walijikuta wanazoeana kabisa, hali iliyopelekea Robert aupoteze kabisa upweke aliokuwa nao, pamoja na woga aliokuwa nao juu ya kwenda sehemu asikokujua na wala kumfahamu mtu yoyote wa huko. Ucheshi alioonesha Vicky muda huo ulimfanya Robert ajikute katika hali ya furaha kama alivyokuwa kwao.
“Umetokea wapi Robert”
“Dar”
“Mhm, Tanzania?”
“Kwani hapa wapi”.
“Kule ndio Tanzania sababu kila kitu kiko huko”
“Hamna hata huku ni Tanzania mbona shule nzuri ziko huku”.
“Lakini Ikulu, Vyuo na hata hospitali nzuri ziko Dar, huduma zote muhimu zipo huko, kule ndio Tanzania bwana”.
“Hapana Vicky hata huku ni Tanzania sio Dar tu”.
Robert aliongea na kisha wote wawili wakaanza kucheka maongezi kati yao yaliendelea tu na huku bado safari yao ikiendelea basi likiwa bado katika mwendo.
“Auuh!”
Robert alilalamika baada ya basi kuwarusharusha pale lilipopita kwenye madimbwi na shimo yaliyokuwepo katika barabara hiyo ya vumbi.
“Hizi ndizo barabara zetu, umeona nimekwambia huku mwishoni mwa Tanzania”.
“Hamna bwana mbona hata Dar kuna barabara kama hizi”
“Kweli!”
“Ehe, zipo nyingi tu tena”.
“Siamini!”
“Kweli na kwambia:
Aliongea Robert na kisha kutabasamu alimwangalia Vicky na baadae kuangalia chini kwa sekunde kadhaa na kuyarudisha tena macho yake usoni kwa Vicky.
“Vipi mbona kimya”
Aliuliza Vicky kwa kudadisi baada ya kuona kama Robert anataka kuongea jambo lakini anasita,
“Hamna kitu, sina story tena”.


E3
“Kwa nini?”
“Basi tu, labda uongee wewe”
“Niongee nini”
“Chochote”
“Haya chochote”
Vicky aliongea na kisha wote wawili walicheka
“Acha utani Vicky ongea chochote”
“Chochote”
Vicky aliongea tena na wakaanza kucheka tena, walicheka mfululizo, kicheko chao kilikatika pale basi lilipoanza kuwarusha rusha tena pale lilipofikia katika eneo lenye  mashimo, watu wote ndani ya basi hilo walikuwa wakilalamikia hali hiyo wakidai wanaumizwa.
lakini Vicky na Robert hawakuongea chochote zaidi ya kuendeleza tena kicheko chao huku wakigonganisha mikono yao ilikuwa ni furaha kwao hali hiyo ya kurushwa rushwa na gari tofauti na wanafunzi wenzao waliokuwemo ndani ya basi hilo ambao walikuwa wakiilalamikia hali hiyo.
“kama rool costal”
“ndio nini”
Ni mchezo wa kupanda kijigari kinachoendeshwa na mashine linapitia misuko suko yote ya barabara unayoijua wakati mwingine kama mnapata ajali vile, linaogopesha sana”
“wee! Sasa kwa nini watu wanapanda”
“ kuchezea hatari hiari ukijua hatari hiyo haiwezi kukuingiza hatarini ni burudani”
“nimeipenda hiyo”
“nini?”
“jinsi ulivyo usema huo mstari,”
“unafurahisha” Robert alicheka kidogo , na mara gari liliwarusha tena, lakini safari hii hiyo haikudumu.
Ilitlia kabisa mara baada ya basi kufikia sehemu zilizomwagwa kifusi ilikuwa karibu na shule ya Manow maeneo ya Lwangwa. Mji mashuhuri kwa soko la gulio na minada.
“Bado kidogo tu tufike”
“Kweli!”
“Yaa”
Aliongea Vicky kwa kujiamini huku akiingiza mkono wake kwenye begi lake baada ya kufungua zipu ya pembeni mwa begi hilo akachukua kalamu na karatasi na kuanza kuandika mambo Fulani katika karatasi hiyo. Robert alibaki anajiuliza nini anachoandika Vicky lakini hakupata jibu.
“ehe chukua”
Vicky aliongea huku akimkabidhi Robert ile karatasi aliyo kuwa akiiandika
“Ya nini!?”
Akauliza Robert kwa mshangao
“My phone number” (Namba yangu ya simu)
“Your phone number!!” (Namba yako ya simu!!)
Aliongea Robert kwa mshangao
“Yaa”
Vicky aliitikia na kumfanya Robert alibaki ameshangaa
“Nilifikiri haturuhusiwi kuwa na simu!’
“Wanakataza ndio lakini hawana ulinzi mkali”
“Umejuaje”
“Nilisoma hapa masomo ya kompyuta  mwaka jana”.
“Ah, kweli?”
“Yaa”
Aliitikia Vicky kwa kujiamini, na kumuacha Robert katika hali ile ile ya kushangaa na hapo hapo wazo la kupata mwasiliano na familia yake lilimjia kwamba angeweza kuwasiliana nao kupitia simu ya Vicky, alipofikiria hilo tu furaha ilimiminika moyoni mwake na kujikuta anashindwa kulizuia tabasamu lililotokea usoni kwake.
“Vipi mbona unatabasamu”
Aliuliza Vicky alipoiona hali hiyo ya furaha usoni kwa Bobert
“ah nimefurahi kujua kwamba una simu”
“mhu”
Vicky aliguna kidogo na kisha kujichekesha kidogo
“Na wewe si unayo”
“Hapana sina”
“ah masihara hayo”
“Kweli nakwambia, Askofu kanieleza simu haziruhusiwi hivyo baba kaichukua na kurudi nayo nyumbani”
“Oh pole sana” aliogea kwa huruma
“Asante”
“Lakini usihofu tutatumia wote hii ya kwangu”
Aliongea Vicky na kumfanya Robert azidi kufurahi kwani alichokiongea Vicky ndicho alichokuwa anatamani kiwe.
“Nitashukuru sana Vicky, utakuwa umenisaidia kweli!”
“Usijali Robert”
Aliongea Vicky huku akitabasamu na Robert alitabasamu pia, macho yao yakagongana kwa sekunde kadhaa pasipo yoyote kati yao kuongea chochote.
“Tumefika!!”
Ilikuwa sauti ya mmoja kati ya wanafunzi waliokuwepo kwenye basi hilo na kuwafanya wenzake wote wachungulie madirishani na ndio hiyo Sauti iliyofanya hali ya ukimya kati ya Vicky na Robert itoweke na kujikuta kila mmoja anayapoteza macho yake usoni kwa mwenzake.
“Kweli tumefika?” aliuliza
“Ehe, ni hapo tu”
Aliongea Vicky huku akiyaonyesha majengo yaliyoonekana upande wa kushoto wa barabara hiyo.
“Shule nzuri, ona mazingira yake yanavyovutia”
Aliongea Robert huku macho yake yote mawili akiwa anayaelekeza kwenye shule hiyo, aliona ni mahali pazuri ajabu.
“Sio  nzuri kwa mazingira tu hata taaluma yake ipo juu”
Vicky aliongea akijaribu kuisikia zaidi shule hiyo, basi lilikwisha ingia kwenye geti ya shule na kuelekea yalipo maegesho ya magari hapo ndipo liliposimama na baadae wanafunzi wote walishuka huku sura zao zikionyesha furaha macho nayo yakiwa juu juu kutizama huku na kule katika mazingira hayo ya shule ya Manow huku Vicky akijaribu kumwelekeza baadhi ya sehemu, aliendelea kuwa karibu hivyo utafikiri walitoka sehemu moja, mpaka walipotengana pale kila mmoja alipoelekezwa mwelekeo tofauti na hata hivyo walipanga kukutana jioni ya siku hiyo ili Robert apate nafasi ya kuwasiliana na ndugu zake. Ni kwa muda huo waliotengana ndio Vicky alipata nafasi ya kukutana na rafiki zake ambapo maongezi yao ya kwanza ilikuwa ni juu ya Robert  marafiki zake wote wawili walitaka kujua ameongea nini na Robert

E4
“Tuambe tu shosti mbona unatubania”
“hamna chochote cha maana yani atujaongea chochote kile”
“masihara hayo, Vicky yani hata mapenzi hamjaongelea”
“Mapenzi wapi ,mtu mwenyewe anaonekana yuko mbali na mapenzi,sijui kwa nini?,lakini nitajua tu jinsi ya kumpanga”
“Lakini unampenda kweli?”
mmoja kati ya marafiki zake Vicky aliuliza,badala kujibu swali Vicky alianza kucheka rafiki zake wakabaki wanashangaa sababu hawakujua kitu kinachomchekesha.
“Unacheka nini sasa?”
“Acha kunichekesha Suzy,kweli yule ndio mwanaume wa kupendwa na mimi?”
Vicky aliongea kwa dharau na kuanza kucheka tena.
“Sasa mbona unataka kuongea nae kuhusu mapenzi!?”
aliuliza tena Suzy  kwa mshangao
“Mapenzi wapi nataka nimwingize kwenye kumi na nane zangu nianze kumchuna pesa,
Si unajua   mtoto wa kibopa yule”
“Da hapo utakuwa umecheza kweli au sio Anita”
,aliongea suzy na kumuuliza yule rafiki yao wa tatu kama wako sambamba.
“kweli”
Anita aliitikia japo kwa kusitasita kisha wote watatu wakacheka huku wakifurahia mpango ambao Vicky anafikiria kuufanya.
waligonganisha mikono yao na kisha kuendeleza kicheko chao.
Jioni kama ilivyokuwa ahadi yao Vicky na Robert waliweza kukutana.Jambo la kwanza baada ya salam Robert aliomba kupatiwa simu.
baada ya kumaliza maongezi yake kwenye simu Robert alibaki na furaha kubwa ambayo ilionekana wazi usoni kwake,
alifurahi sana kuongea na familia yake alijiona kama vile yupo pamoja nao.
“Umefurahi?”
Vicky alimuuliza  wakati Robert akijichekesha peke yake kutokana na furaha aliyokuwa nayo
“Sana nashindwa jinsi ya kuielezea furaha hii”
“Sasa nataka kuifanya furaha yako iwe mara mbili”
“What?,oh,no way , you can’t Vicky”[Nini?, oh hapana Vicky huwezi]
Aliongea Robert huku sura ikiwa bado imejawa na furaha
“Sikiliza Robert nasema hivyo sababu jambo moja ambalo nataka kukueleza leo  tena sasa hivi”
“Sasa hivi?”
Robert aliuliza
“ndio”
Vicky aliitikia
“kitu gani hicho?”
Robert aliuliza kwa mshangao huku akimuangalia usoni ambapo Vicky nae alimkazia macho Robert kweli kweli kama vile mtu mwenye hisia kali na kisha akaanza kuongea katika hali isiyo kuwa ya utani kabisa.
“Huu ndio ukweli Robert mimi nakupenda, nakupenda kuliko kitu chochote kile katika hii dunia  naomba uamini nachosema”
Aliongea Vicky bila kusita huku bado akiwa amemkazia macho Robert, ambae mara baada kusikia kauli hiyo mapigo ya moyo wake yalibadilika na kuanza kudunda kwa kasi  huku tabasamu lililokuwepo usoni kwake likipotea taratibu, aliitafakari kauli hiyo ambayo hakutegemea kabisa kuisikia tena toka kwa msichana mrembo kama Vicky. Hakutegemea kabisa kwamba kuzoeana  na Vicky kungemfanya ajikute kwenye dimbwi la mapenzi hakutegemea kabisa hata kwa ndoto ya kuwa siku moja angekuwa na msichana mrembo kama Vicky. Tabasamu lilivamia ghafla usoni kwake na kujikuta anapagawa kwa furaha na kuifanya furaha yake iongezeke na kuwa mara mbili zaidi ya ile aliyokuwa nayo mwanzo
“Umeweza Vicky umeweza kweli kuizidisha furaha yangu,nakupenda Vicky nakupenda pia”
Aliongea Robert kwa furaha na kujikuta anamkumbatia Vicky kwa furaha
“nakupenda sana Robert”,
aliongea vicky
“Hata mimi nakupenda”
Robert alizidi kusisitiza huku bado akiwa amemkumbatia Vicky huku wakiwa wamejisogeza kwenye giza totoro.
Mapenzi yao yakawa huku kila mmoja akionyesha kupagawa kabisa na penzi la mwenzake  zaidi ilikuwa kwa Robert ambae alikuwa kama vile mwendawazimu.
Alikuwa tayari kwa lolote alikwisha jitoa mhanga kwa ajili ya penzi hilo, bila kujua kwamba Vicky hakuwa pamoja bali alikuwa akifanya maigizo na sio mapenzi ya kweli kama ambavyo Robert alivyokuwa akifikiria.
“Vicky”,
Robert aliita
“Mh”
aliitika
“Nakupenda kuliko kitu chochote kile”
“Hata mimi nakupenda dear”
“Nakuamini na najua utakuwa na mimi siku zote”
“Usihofu kabisa kuhusu hilo,mimi nimezaliwa kwa ajili yako”
“hata mimi kwa ajili yako mpenzi” Robert aliitikia wakiwa wameketi gizani usiku mmoja,
hakujua chochote kilichoendelea moyoni kwa Vicky ,alichojua yeye ni kwamba ana bahati kubwa kuwa na msichana mrembo na mwenye uzuri wa aina yake .hakufahamu kabisa kitu kilicho mvutia Vicky kwake
“am a lukiest man in the world!” ( mimi ni mwanaume mwenye bahati zaidi ulimwenguni!)
aliwaza Robert akiwa na imani kabisa kwamba amepata zali kama lile la mentali , bila kujua kwamba yumo ndani ya mtego.

***********-********-*********-*********

Kwa Vicky na marafiki zake furaha ilitawala kitendo cha Vicky kumpata Rober kilikuwa ni ushindi mkubwa sana kwao.
Sio kwamba walifurahia Vicky kupata mpenzi la hasha bali kwao uhusiano wa Vicky na Robert, ilikuwa kama vile Vicky amechimba mfereji wa pesa hivyo pesa zingekuwa zikimjia tu kama mvua.
Na kweli jambo hilo lilifanikiwa kwa kiasi kikubwa kwani Robert hakujisikia furaha bila kumpatia hela Vicky , aliamini kwamba Vicky ndio mtu pekee mwenye uhalali wa  kutumia fedha anayotumiwa na wazazi wake aliamini hivyo sababu alimchukulia Vicky kama ubavu wake sababu yeye ndio msichana pekee katika dunia aliyetokea kumpenda.
Alimpenda sana alimchukulia kama malkia wa moyo wake na hakutegemea wala kufikiria kwamba  anaweza kumpenda mwanamke mwingine kama anavyo mpenda Vicky.
“I will love you forever baby” (Nitakupenda milele mpenzi)
,aliwaza Robert huku akimwangalia Vicky kwa hisia kali.aliamini hakuna mwanamke anayeweza kuchukuwa sehemu kubwa ya moyo wake kama ilivyo kwa Vicky.
Aliamini Vicky ndio msichana pekee anae upendeza moyo . Hakuja lililopo moyoni kwa Vicky,hakujua kabisa kwamba Vicky  anamchukulia yeye kama mpira alioutoboa kwa sindano ili kuufanya utoe upepo taratibu .hakujua kwamba  VICKY  yupo kwake sababu ya pesa na sio mapenzi kama anavyo muongopea.
Siku moja katika makutano yao ya kila siku Vicky alionekana mnyonge hali hiyo ilimshtua sana Robert  alitaka kitu kilicho mpata mpenzi mpaka awe katika hali hiyo ya huzuni namna hiyo, hakusita kumuuliza japo alikuwa na wasiwasi sana moyoni,kwa zaidi ya dakika kumi na tano alikuwa akimbembeleza Vicky ili amweleze ni kitu gani kinacho mfanya awe katika hali hiyo ya unyonge lakini Vicky alikuwa  mgumu kutoa jibu , kitendo hicho kilizidi kumchanganya Robert na kumfanya azidi kuingiwa na wasiwasi.
Alizidi kumbembeleza lakini ugumu wa Vicky uliendelea hali ilizidi kuwa mbaya kwa Robert ambae sasa alianza kulengwa na machozi
“Nina matatizo Robert”
mwishoe Vicky aliamua kuongea
“matatizo gani niambie mimi eh ni nini?”
Robert aliuliza kwa sauti ya upole na ya kubembeleza, kwa kujivuta Vicky akajibu
“Nataka kuuza simu !”
“Uuze simu!! , kwa nini?”
aliuliza Robert kwa mshangao
“Ndio maana nimekueleza kwamba nina matatizo”
“Matatizo gani hayo dear mbona hutaki kunieleza!?”
aliuza Robert kwa sauti ya upole
“We acha tu mpenzi wangu yani makubwa”
“We nieleze tu hata yaweje”
“Nadaiwa shilingi elfu thelathini na suzy ,toka muda mrefu nilikuwa nikimzungusha lakini leo amenibana anataka nimpe hela yake leo leo”
aliongea Vicky kwa huzuni
“Yani hilo tu ndio linakuumiza kichwa sasa hukunieleza toka mwanzo!?”,
aliongea Robert kwa mshangao kwani kwani hakuona kwamba hilo linaweza kuwa tatizo la kumfanya mpenzi wake auzunike kiasi hicho
“Nilijua labda na una mambo yako”
“Mambo yangu yapi Vicky, wewe ndio mambo yangu, shida zako zote nizakwangu”
aliongea Robert na kumfanya Vicky ainamishe macho yake chini kwa aibu moyoni dhamiri yake ilimsuta sababu alichokiongea kwa Robert ulikuwa ni uongo mtupu shida yake ilikuwa pesa tu
“Popote utaponiona ujue nipo kwa ajili yako , nakupenda Vicky”
aliongea Robert  na kisha kushika kidevu cha Vicky na kumuinua.
macho yao yaligongana Vicky aliyayumbisha macho yake nakujikuta anagota kwenye mkono wa Robert  alipoziona noti tatu za shilingi elfu kumi kumi zikiwa kwenye mkono huo.Alihisi mate yamemjaa mdomoni kwa tamaa furahaa ya ghafla ilifurika moyoni kwake . alishindwa kuongea chochote akabaki akihemahema huku machozi ya furaha yakimbumbujika.
“It’s for you baby” (Hii ni kwa ajili yako mpenzi)
Robert aliongea kwa sauti kunon’gona huku akimkabidhi Vicky noti hizo .
Bila kutegemea Vicky alijitupa mwilini kwa Robert nakumkumbatia huku akiongea maneno mengi mengi ya kimapenzi
“Nakupenda Robert,nakupenda toka moyoni!”
Vicky aliongea maneno hayo yaliyomfanya Robert azidi kupagawa kwa furaha na kujipa uhakika wa kuwa na Vicky katika maisha yake yote.

******---********---*********---**********--*******

Mapenzi yao yalikuwa wazi sasa karibu kila mwanafunzi wa shule hiyo alijua kwamba Robert na Vicky ni wapenzi na wako kwenye mapenzi mazito.
Kasoro Anita na Suzy marafiki wakubwa wa Vicky ndio walijua ukweli halisi wa penzi hilo, walijua kwamba Vicky yupo kwa Robert sababu ya pesa.
Penzi liliendelea huku Robert akizidi kupagawishwa na penzi hilo, karibu muda wote alimfikiria Vicky, alikuwa bado haamini kwamba Vicky anaamini kwamba yeye anampenda kweli kweli .Alitaka kumsibitishia Vicky juu ya penzi la dhati lililopo moyoni mwake lakini hakujua angefanya hivyo kwa njia gani, alipokuwa katika hali hiyo kufikiria ndipo alipopata wazo ambalo aliona lingeweza kutatua tatizo hilo.
Aliamua kumpigia simu dada yake na kumtambulisha Vicky kwake aliamini kwa kufanya hivyo angeweza kumfanya aamini kwamba kweli anampenda kwa dhati.
Ajawahi hata siku moja kumweleza dada yake habari za mapenzi lakini siku hiyo ilimbidi ilikudhibitisha penzi la dhati alilokuwa nalo kwa Vicky. Alipiga simu
“Hallow Dada , vipi huko wazima!”.
Aliongea Robert muda mfupi baada ya simu kupokelewa
“Safi tu mdogo wangu ,vipi wewe mzima!?”
ilsikika sauti ya upande wa pili
“Mi mzima tu Dada!”
“Unaendeleaje na masomo?”
“Salama tu Mungu anasaidia,Baba na mama wazima?”
“Wazima tu yani hakuna tatizo kabisa”.
“Dada nina habari mpya”.
“Zipi hizo!?”
“Kuhusu mimi”
“Nini?”.
“Nina mpenzi sasa!”.
“Mpenzi!!!”
“ndio Dada anaitwa Vicky tunapendana sana!”
“Hongera zako”
“Asante, yupo hapa nataka uongee nae”
“mpe simu basi niongee nae wifi yangu”
“haya huyu hapa”
“Shikamoo”
Vicky alisalimia
“Malhaba Vicky hujambo!”
“Sijambo!”
Vicky aliitikia
“Nimefurahi kuku fahamu Vicky , niambie kweli unampenda mdogo wangu?”
Rehema dada yake Robert aliuliza swali hilo
na kutega sikio lake kwa makini iliasikie jibu atakalopewa na Vicky
“Ndio dada nampenda sana”
Vicky aliitikia haraka haraka
“Kweli?”
Aliuliza tena
“Kabisa” aliitikia
“Nimefurahi kusikia hivyo, ila naomba uniahidi kitu kimoja”
“kitu gani?”
“Niahidi kwamba hautamuumiza mdogo wangu”
“Nakuahidi”
“ahsante sana”
“Na wewe pia”
“Haya mpe simu Robert”
“Sawa kwaheri”
“Hallow dada”
“Robert japo sijamuona lakini nahisi Vicky ni msichana mzuri hongera kwa kuchagua”
“Asante dada!”
“Okey bye!” ( sawa kwa heri! )
“Bye!”  ( kwa heri )
Robert aliitikia na kisha kukata simu, moyo wake ulikuwa umejaa furaha tupu,
alifurahishwa sana na kitendo cha Rehema kumfurahia Vicky na pia alifurahia kitendo cha kufanikisha lengo lake la kumsibitishia Vicky kwamba kweli anampenda kwa dhati.
“Umeamini vicky umeamini kwamba kweli nakupenda eh!”
“Robert mimi nakuamini , nakuamini kwa asilimia zote naomba usiwe na wasiwasi kabisa”
“Kweli Vicky!”
“Kabisa”
Vicky aliongea na kisha kumsogelea Robert
“Mwaa!”
alimbusu Robert shavuni, busu hilo lilifika mpaka moyoni kwa Robert na kumfanya azidi kupagawa na penzi hilo na kujiona yupo katika dunia ya peke yake , yeye naVicky tu kama ambavyo Adam na Eva walivyokuwa katika bustani ya Edeni.

Vicky alizidi kufurahi pale alipoona Robert anazidi kuchanganyikiwa na penzi. Akiamini kwamba hali hiyo ingemfanya awe na uwanja mpana wa kupata pesa toka Robert ambae alikuwa tayari kuongea kila aina ya uongo kwa wazazi wake ili waweze kumtumia pesa zaidi ili aweze kumpatia Vicky.
Vicky aliwasimulia rafiki zake juu ya hatua ya Robert kumtambulisha kwa dada yake
“Nikamwamkia akaitikia ,akasema nimefurahi kukufahamu ,akaniuliza kama kweli nampenda mdogo wake nikamjibu ndio na tena akaniomba nimuahidi kwamba sito muumiza mdogo wake pia nikamuahidi”
Vicky alimaliza kuongea kauli hiyo na kuanza kucheka ambapo suzy nae akaanza kucheka pia.
“Umempatia kweli,saizi utakuwa unachuna kotekote”
Suzy aliongea na kisha kuendeleza kicheko pamoja na Vicky.
Tatizo lilikuwa kwa Anita ambae tangu walipoanza mazungumzo hayo mpaka muda huo yeye alikuwa amebaki kimya tu .kitendo hicho kiliwafanya Vicky na Suzy wabaki wakimshangaa kwani hiyo haikuwa kawaida yake.
“Vipi Anita mbona hivyo!?”.
Aliuliza Vicky kwa mshangao
“Siwezi kuendelea kuunga mkono huo ubaya wako”
“Ubaya gani !?” ,
Vicky aliuliza huku bado akiwa katika hali ya kushangaa ,hakuelewa kabisa kitu ambacho Anita anakizungumzia.
“Ukatili huo unao mfanyia mtoto wa watu!”
aliongea Anita kwa ukali
“Ukatili!!”.
“Ndio ukatili, huwezi kumchezea mtoto wa watu kiasi hicho”.
“Mbona sikuelewi Anita!?”
“Unielewi nini unavyomuongopea Robert unafikiri huo sio ukatili eeh, amekukosea nini mtoto watu mpaka umfanyie yote hayo!?”.
Anita aliongea kwa ukali huku Vicky na Suzy wakiwa midomo wazi kwa mshangao hawakutegemea kabisa kwamba Anita angediriki kuongea maneno kama hayo mbele yao.
Ilikuwa ni ajabu kweli kwao kwani Anita ni rafiki yao lakini sasa ameonyesha moyo wa usaliti
“anita kama mimi namuongopea Robert wewe inakuhusu nini?”
aliuliza Vicky kwa ukali
“Hata kama hainihusu lazima nikwambie ukweli umezidi Vicky”
Anita alijibu kwa kufoka, Vicky alifoka na Anita alifoka pia yani hakukuwa na maelewano kabisa.
“Kama mimi nimezidi sasa wewe sasa inakuhusu nini?”
“Hapana Vick….”
Suzy alimkatisha
“Hapana nini Anita wewe hayo haya kuhusu ni mambo ya Robert na Vicky we unaongea kama nani?”
Suzy nae alifoka
“Suzy na wewe unamuunga mkono!?”
aliuliza Anita kwa mshangao, alimshangaa Suzy sababu yeye ndio alikuwa mtu wa kwanza kumteta Vicky karibu kila siku Vicky alipokuwa mbali nao akidai Vicky anafanya vibaya huku akilaani kitendo hicho lakini ajabu katika kumweleza Vicky ukweli anaamua kugeuka kama kinyonga na kujifanya yuko upande wa Vicky
“Sasa kumbe ulifikiri mimi ni msariti kama wewe, unajifanya rafiki kumbe una lako moyoni mnafiki mkubwa we!”
aliongea Suzy kwa nyodo.
“Na kwa taarifa yako hatuiitaji kampani yako tena na ukijifanya unaleta kidomodomo chako tuta kufunza adabu!”
Vicky aliongea kauli hiyo kwa ukali akijaribu kumtisha Anita , sababu alihisi kwamba Anita anaweza kumweleza Robert ukweli.  Jambo Vicky hakutaka litokee kabisa kwani lingemfanya akose  hela ambazo alikuwa anazipata kwa kumchuna Robert. Anita alitishika na maneno ya Vicky sababu alilijua balaa lake akitibuliwa,ujasiri wote aliokuwa nao ulimwisha akabaki kimya kwa nukta kadhaa huku uso wake ukionyesha wazi wasiwasi aliokuwano.
Lakini hata hivyo hakutaka kuishia hapo moyo wake ulimsukuma kuongea zaidi
“Poa tu hata mkinitenga ,lakini mambo hayo lazima yawatokee puani”.
Aliongea Anita kwa wasiwasi huku akirudi nyuma ambapo aligeuka nyuma kuanza kuondoka haraka aliogopa kupigwa kwani alijua Vicky ana uwezo huo .
“Eti yatatutokea puani mjinga kweli huyu!”
aliongea Vicky huku akimcheka  Anita ,walicheka pamoja na Suzy huku wakigonganisha mikono yao hawakujali tena urafiki wao na anita , sababu anita alishawaasi na kuwasaliti.
***

MWISHO WA KITABU CHA KWANZA



1 comment:

  1. Инстраграмм являться самой популярной на данный момент площадкой для продвижения своего бизнеса. Но, как показывает практика, люди гораздо чаще подписываются на профили в каких уже достаточное количество подписчиков. В случае если заниматься продвижение своими силами, потратить на это можно очень немало времени, потому гораздо лучше обратиться к спецам из Krutiminst.ru подробнее https://fxprimer.ru/index.php?topic=18008.14745

    ReplyDelete