GIFT KIPAPA

Friday, July 8, 2016

MKE WANGU ANATAKA KUNIUA BOOK 1





By gift kipapa
KWA UFUPI;
Utafanya nini endapo ukigundua kwamba Yule unayempenda na kumthamini kuliko kitu chochote cha maisha yako, ndio mtu hatari zaidi kwako , unalala nae kitanda kimoja, na unamshirikisha maswala yako yote lakini pale inapofikia hatua ya mtutu wa bunduki kunyooshewa kwenye paji la uso wako ni yeye ndio anakuwa amekishika kifyatulio cha risasi, hafanyi mzaha na wewe , bali ni kweli kabisa  amenuia kukumaliza bila shaka hicho kinaweza kuwa kipindi kigumu zaidi katika maisha yako, simulizi hii iliyonuia kuugusa moyo mmoja hadi mwingine  imesukwa kwa mara nyingine  na Deogratius gift kipapa Lwasye ili kuongea na moyo wa yoyote huko nje ambaye yupo katika uhusiano wa kimapenzi na hata aliye nje ya uhusiano.
MWANZO WA SIMULIZI:
Ni miezi miwili tu imepita tangu nifunge ndoa. Harusi kubwa ya kifahari iliyokuwa imesheheni kila aina ya vivutio. Mbali na hayo harusi hiyo kwangu ilikuwa kutimilika kwa ndoto ya kukamilisha furaha katika maisha yangu kwa kuoa mwanamke mwenye kila sifa ya uzuri  ambao nilikuwa nataka mke wangu awe nao, alikuwa mzuri sio siri machoni pangu alionekana kama vile malaika , na kweli  alikuwa , nilipokutana naye kwa mara ya kwanza niliamini ni Mungu mwenyewe ndio ameamua kunishushia mrembo huyu. Jina lake ni judy , lakini mimi nilipenda kumuita malaika.
“malaika wangu.”
“abee , mume wangu.”
Aliitika.
“nakupenda sana.”
“Nami nakupenda pia mume wangu.”
Hivyo ndivyo mapenzi yetu yalivyokuwa , tulipenda na sana sio siri.
Baada ya kufunga ndoa yetu tulienda kula fungate yetu nchini Thailand  katika jiji la bangkonk. Jiji lililosheheni kila aina ya starehe. Tukiwa huko siwezi kukuficha jinsi maisha yetu yalivyokuwa ya furaha.
Tulitembea katika jiji hilo kama malkia na mfalme tukifurahia vivutio vya mji huo pamoja na kwenda kwenye vivutio vya kila aina kama vile maporomoko ya maji ya kushangaza na  fukwe za bahari zilizo sehemu iliyojificha na mambo mengine mengi ambayo hata kuyaelezea siwezi , kwa kweli ilikuwa furaha tupu. Mpaka tulitamani maisha yetu yote yangekuwa huko.
“mume wangu , yani nimepapenda kweli hapa.”
“hata mimi mpenzi lazima tutakuja tena rikizo.”
“kweli?”
“niamini  mke wangu.”
“nitashukuru kweli mume wangu yani.”
“usihofu mpenzi wewe ni malkia wangu , nitafanya kila kitu , kwa ajili yako.”
“ndio maana nakupenda honey .”
Aliongea na kisha kunibusu , na wala halikuwa busu rahisi bali denda , macho yetu yalifumba tulipokuwa tunyonyana , wala hatukuogopa kufanya hivyo barabarani kwenye umati wa watu waliokuwa wametingwa wakihangaika na shughuli zao hakuna hata aliyekuwa na muda wakutuangalia sisi.
“habari , ndege wawili , mnataka kunywa  damu ya nyoka .”
Aliongea mwanume mmojamwenye asili ya huko  aliyesogea karibu yetu na kutufanya tukatishe busu letu.
“damu ya nyoka!”
“ndio damu ya nyoka ,kobra, sssssss.”
Aliongea huku akijaribu kuuchezesha ulimi wake na kutoa sauti ambayo nyoka huwa wanatoa  wakiwa wameutoa ulimi wao.
 “hapana , hatuhitaji damu ya nyoka.”
Niliongea .
“kwa nini mnaogopa , wapendanao wengi wanapenda kunywa, inasemekana mkinywa damu ya nyoka kwa pamoja mnafanya mapenzi yenu yadumu kwa muda mrefu zaidi.”
Aliongea mwanaume huyo huku akituangalia usoni.
Na sisi pia tuliangaliana usoni , kusema kweli hoja yake ilikuwa imetugusa sote , hatujawahi kunywa damu ya nyoka na wala hakuna yoyote kati yetu aliyewahi kufikiria kama siku moja atakuja kunywa kitu kama damu ya nyoka , lakini kwa ajili ya mapenzi , kwa kweli mtu anaweza kufanya lolote.
“tutakunywa!”
Tulisema kwa pamoja hadi wenyewe tulijishangaa , kugongana sauti , mwanaume huyo alitupeleka kwenye chumba hicho ambacho walikuwa wakiiandaa hiyo damu ya nyoka , karibu chumba kizima kilikuwa kimejaa nyoka aina ya kobra na wengine tofauti tofauti.

Lakini walikuwa katika masanduku ya vioo ,na katika masanduku hayo muda wote walikuwa wakitishia kung’ata mtu yoyote aliyeingia kwenye chumba hicho japo waliishia kuvigonga vioo vya masanduku hayo.
“kwenye meza ya kupimia hiyo damu ya nyoka kulikuwa na mwanaume mwingine ambaye alimimina damu hiyo kwenye .
Kweny glasi ndogo zile zinazotumika kunywea pombe kali baa.
Tulishika glasi hizo huku tukiangaliana usoni .
“kwa ajili ya mapenzi yetu.”
 Niliongea huku nikimsogezea Judy  glasi hiyo ili tugonge chears.
“kwa mapenzi yetu.”
Naye pia aliitikia  na kisha tuliyagongesha maglasi hayo na kunywa kwa pamoja .
Sio siri damu hiyo ilIkuwa chungu, lakini ilitubidi tumeze hivyo hivyo.
Hivyo ndivyo yalivyokuwa mapenzi yetu huko Bangkok ,  na sasa tupo nyumbani tanzania kwenye makazi yetu Mbezi beach , wiki moja imesha pita tangu tuwasili kutoka nchini Thailand
***
  Ndugu jamaa na marafiki walitupokea kwa shangwe tuliporejea nchini. Ilifanyika sherehe kubwa nyumbani kwetu, na baadae sherehe iliamia katika ukumbi wa Diamond Jubilee.
Yani harusi ni kama vile ilikuwa imefungwa upya, ndugu zangu wote walirejea nyumbani tena kwa ajili ya kuja kunipokea mimi pamoja na mke wangu , japo nao pia walikuwa wanatoka nchi mbali mbali, ulikuwa ni utamaduni ya familia yetu.
Hata ukiwa mbali kiasi gani na uwe umetingwa kaisi gani, ikifanyika shughuli nyumbani basi lazima uhudhurie, baba yabgu alikuwa mkali sana kwa yoyote anayethubutu kukosa kuhudhuria.
Hata hivyo tofauti na shughuli zingine zilizowahi kufanyika katika familia yetu, hii ilionekana kuwafurahisha zaidi ndugu zangu , nafikiri  kwa kuwa nilikuwa mziwanda na kipenzi cha kila mmoja hata hivyo  hii ilikuwa harusi ya mwisho kufungwa katika familia.
Kaka zangu wote pamoja na dada tayari walikuwa wamefunga harusi zao , kama miaka mitano sita hivi iliyopita na wengine walikuwa mpaka na miaka kumi na tano katika ndoa.
Ukumbini niliwaarika wafanyakazi wangu wote, siku hiyo ofisi haikufunguliwa kabisa , kila mmoja alikuwa hapo kusherekea kurejea kwa bosi.
 Na wana familia walichokifanya siku hiyo kilikuwa cha kushangaza kwa kweli , walianza kutoa zawadi upya kila mmoja alitoa zaidi ya zile zawadi alizotoa siku ya harusi , ilikuwa ni kufuru kwa kweli , magari ya kifahari tulimiminiwa kama vile utitiri , yani kama vile tulikuwa tunapewa mtaji wa kuuza magari.
Na mama yangu ndio alitia fora zawadi aliyoitoa ilifunika zawadi zote zilizotolewa siku hiyo na kufanya watu wote washikwe na bumbuwazi.
“sitaki mwanangu ajibane bane tena atakapokuwa anasafiri , ndege hii binafsi ataitumia katika safari zake zote akiwa na mkewe.”
Aliongea mama na watu wote walishangilia , mimi mdomo wangu ulikuwa wazi , nilijua kwamba mama ananipenda kuliko watoto wake wote lakini sikujua kwamba angeweza kudiriki kuninunulia ndege yangu mwenyewe .
Ilikuwa ni model mpya kabisa ya ndege ilikuwa ni ndege ya kifahari yenye injini mbili model: the new eclipse 550 personal jet.
Gharama yake ilikuwa ni dola milioni 2.7 na ilikuwa na inakadiriwa kwenda kasi mpaka mph 430.
Hata baba mwenyewe alishangazwa na zawadi hii , pamoja kushinda nae lakini siri hii hakumwambia.
Ndugu zangu wote walibaki wameduwaa. Na kwa mke wangu ndio ilibaki kidogo azimie kwa mshtuko jambo hili lilikuwa limepitiliza kusema kweli.
Na ilipofika zamu yangu ya kuongea chochote kwa watu.
Nilishika kipaza sauti huku nikijidai. Maneno yangu yalikuwa machache lakini yalimgusa kila mtu.
“ninapaswa kuwashuku watu wote mliopo hapa, lakini mniwie radhi kwa kile ambacho mama yangu amefanya leo kimeziteka hisia zangu zote. Amenifanya nitambue ya kwamba yeye si mwanamke aliyebeba kwenye tumbo lake na kisha kunizaa na kunilea mpaka nilipokuwa mtu mzima na kunicha niende zangu, leo amenithibitishia kwamba ni mwanamke mwenye uwezo na nguvu za kunilinda katika kipindi chote cha maisha yangu, ni wangapi kati yenu hapa mama zenu wanaweza kufanya hivyo  mnyooshe mikono yenu ili niione.”
Nilipoongea hivyo kuna baadhi ya watu walinyoosha na wengine walibaki kushangilia tu.
“msidanganye, msidanganye! Sijauliza kwamba wangapi wanapendwa na mama zao, najua kila mama anampenda mwane ,  nimeuliza ni wangapi mama zenu wana nguvu kama alizo nazo mama yangu, na nitakuamini kama ukinionyesha ndege ya kwako mwenyewe , ambayo umezawadiwa na mama yako. ”
Niliongea huku watu wakicheka , kwa kweli siku hiyo ilikuwa siku ya kipekee kwangu.
Marafiki ndugu zangu na wafanyakazi wote wa kampuni yangu walikuwa na furaha kweli siku hiyo, tulikunywa kadiri tulivyojisikia , tulicheza muziki na kusherekea kwa kila namna , kwa kweli siku hiyo ilikuwa siku kweli kweli.
Ahsubuhi ya siku iliyofuata wafanya kazi wangu hawakwenda kazini niliwaamuru wapumzike.
mgazeti yaliyochapwa siku hiyo yalipabwa picha yangu. Huku yakiwa na vichwa vya habari vilivyoeleza kunihusu , kila gazeti waliandika kichwa hicho kwa kukipamba kwa jinsi walivyojua wao.
‘ TAJIRI DEO AREJEA JIJINI’  ‘ DEO AFANYA KUFURU’    ‘JIJI LAWAKA MOTO KWA MBWE MBWE ZA DON DEO.’
 na vingine vingi wala sikujali picha yangu kupabwa kwenye magazeti lilikuwa jambo la kawaida , nikionekana kwenye kumbi za starehe , nikitoa msaada Fulani , nikishinda tenda , nikiwa mgeni rasmi kwenye hafla Fulani na hata wakati mwingine nikionekana katika maeneo ya uswahilini, wenyewe waliniita Don lakini
nina hakika watu hawa hawajui lolote kuhusu ndugu zangu, kwani kila kitu nilicho nacho kilikuwa ni taka taka tu kwao.
 Hawa watu waliandika chochote kuhusu mimi na watu walinunua magazeti yao.
“honey , umependeza kwenye hili gazeti.”
Aliongea mke wangu akionyesha picha iliyokuwa kwenye moja kati ya magazeti yaliyokuwa mezani. Ilikuwani picha tuliyokuwa wote  wawili tikiwa tumekumbatiana.
“mbona hata wewe umependeza malaika wangu.”
Nilimuitikia .
“No honey yako ndio nzuri zaidi.”
Aliongea Judy kwa kudeka.
“okey sawa sitaki kukuuudhi malaika wangu, nimekubali mimi ndio nimependeza zaidi.”
Niliongea kwa kumbembeleza.
***
Nae alisogeza kichwa chake na kuniegamia nikawa na kikuna kuna kichwa chake ,
“nimekudanganya.”
Niliongea .
“nini ?”
Aliuliza kwa mshtuko.
“wewe ndio umependeza kuliko mimi.”
Niliongea na kisha nikicheka , alichukua mto uliokuwa kwenye sofa na kuanza kunipiga nao .
Niliiinuka kwenye sofa hiyo  huku nikikimbia , alinikimbiza huku akicheka , tulikimbizana  huku yeye akiwa ameushika ule mto ili anipige nao tena pindi atakaponikamata.
“oh , oh.”
Nilalamika pale aliponikamata. Shati langu
“I will kill you!  I will kili you!”
[ nitakuua nitakuuua.]
Aliongea huku akinipiga piga na mto.
“sawa mpenzi nimekoma , nimekoma sirudii tena .”
Nilijaribu kujitetea lakini yeye aliendelea kunipiga na mto huo .
Nikaudaka  na kufanya ashindwe kunipiga nao tena alijaribu kuuvuta toka kwangu lakini alishindwa sababu nilikuwa na nguvu kumzidi.
Aliuachia mto huo kinyonge na kisha kuondoka hapo akikimbia, macho yake yalikuwa yamelengwa na machozi , muda wowote angeweza kukudondosha machozi.
“honey, am sorry, honey please wait for me.”
Niliongea huku nikimkimbilia, haraka haraka alikuwa akipanda ngazi sikuweza kubahatika kumdaka popote mpaka anamaliza ngazi hizo mimi bado nilikuwa sijamfikia .
Aliingia chumbani na kwenda kujitupa kitandani .
Na kisha kuanza kulia kwa kwa kwi kwi.
“mpenzi tafadhari , usinikasirikie, nakupenda.”
Niliongea kwa sauti ya upole , wakati huo nilikuwa naogopa hata kumgusa, chochote nilichokifanya kilichomfanya hadi adondoshe machozi kwa wakati huo kilikuwa kikinihuzunisha na mimi , kwa kweli sikutamani kabisa kuyaona machozi kwenye uso wa mpezni  wangu, yeye ni malaika , hastaili kulia , kitu pekee nilichotamani kukiona kwenye uso wake ni tabasamu pamoja na zile dimpo zinazoonekana kwenye mashavu yake pale anapotabasamu.
Lakini sio machozi , oh hapana.
“honey , sikunuwia kukutoa machozi , tafadhari  naomba unielewe nakupenda .”
Niliongea huku nikisogea pale kitandani taratibu, nilinyoonya mjkono wangu taratibu ili angalau niiguse ngozi yake , sikujua ni njia gani ambayo ingeweza kumfanya atulie, lakini mikono yangu ikishika angalau mabega yake  nilitumaini pengine hilo linaweza kumfanya ajisikie vizuri.
“sikuhitaji Deo , nenda zako, kaa mbali na mimi.”
Aliongea huku akiendelea kulia akiwa amejilaza kifudi fudi.
Kusema kweli kauli hiyo iliniumiza hata zaidi , nilikuwa makini sana na vitendo vyangu sikutaka kufanya lolote ambalo lingemfanya akasirike hivyo lakini ili jambo nililolifanya nikiwa na nuwia kumfurahisha zaidi limegeuka kuwa jambo la kumhuzunisha. Na sasa kitu pekee nacho kitaka kutoka kwangu si faraja , bali nikae mbali nae.
Sikuwa na kipingamizi niliinuka kwenye kitanda hicho kinyonge na kuanza kupiga hatua , nilipiga hatua ya kwanza ya pili ya tatu nikashtukia ghafla nakumbatiwa kwa nyuma , alikuwa ni yeye , nilihisi joto lake, ngozi yake laini vyote kwa pamoja vilileta furaha ya ghafla moyoni mwangu.
“usithubutu kunyanyua mguu huo na kupiga hatua nyingine , Deo, sababu ukifanya hivyo, naapa nitakuua.”
Aliongea Judy kwa sauti yake laini ambayo kila wakati nikiisikia katika ngoma za masikio yangu nilikuwa nikisisimka kwa hisia , ilikuwa kama melodi nzuri ambazo muda wote zinaupa faraja moyo wangu.
Alinigeuza nyuma na nikageuka kumuangalia , ni kweli macho yake yalibadilika rangi sababu machozi yaliyokuwa yanamtoka , lakini uso wake jinsi ulivyokuwa na tabasamu pamoja na zile dimpo kwenye mashavu yake , zilinifanya nijisikie kwamba mimi ndio mwanaume mwenye bahati zaidi duniani.
Kwa sababu mashavu haya hayakuwa mazuri kwa kuyaangalia tu , bali pia kuyashika na kuyabusu.
“kamwe siwezi kukuruhusu ukae mbali na mimi deo.”
Aliongea maneno hayo kwa hisia huku akiniangalia usoni , naweza kukwambia bwana , macho yangu hayakupepesa kuangalia mahali popote pale zaidi ya kuyaangalia macho yake , kwa sababu pale nilipoyaangalia macho yake nilijiona mimi nikiwa ndani ya macho yake na hicho ndicho kitu kizuri zaidi nilichpenda kukiona katika maisha yangu.
“hata mimi siwezi kukuruhusu uniache mwanadani wangu.”
Nami pia niliongea kwa hisia , kumbatio la sasa lilikuwa ni la nguvu zaidi kila mtu alikuwa akilihisi. Na vile mikono yetu ilivyokuwa ikipapasa maungo yetu basi kila kitu kikabadilika kwa wakati huo na kuwa kitu kingine kabisa , midomo yetu ilikuwa karibu na ndimi zetu ziligusana , na halafu hakukuwa na nafasi ya sisi kusimama tena , tuliikuta miili yetu ikiwa juu ya kitanda , mito ilidondoka chini  na hata mashuka yalitanduliwa , ulikuwa ni mgalo galo tu juu ya kitanda hicho mara tuwe kwenye kona hii ya kitanda mara  ile ,sijui miguu ikishuka chini ya kitanda kichwa kikining’inia , yani lolote lilifanyika ili mradi tujisikie burudani zaidi.
***
Juma tatu siku ya kwanza kuanza kazi tangu nilipo niliporejea nchini , nilipoingia ofisini kitu cha kwanza kufanya ilikuwa ni kuweka picha yetu ya harusi mezani kwangu.
Na kisha nikaitisha kikao cha idara zote ili nijue kilichokuwa kinaendelea ofisini  wakati wote nilipokuwa kwenye fungate langu.
“mikataba miwili imeingia bosi kampuni ya Bikok toka johnseburg, Afrika kusini. pamoja na Khc kutoka Nairobi Kenya.”
“mliwaeleza kuhusu harusi.”
“ndio na wakasema watavumilia, Bikok imekutumia na zawadi pia, lile bmw lililotambulisha na Bw.Maziku unalikumbuka ?”
“ah sio rahisi , bmw zilikuwa ngapi unafikiri ? nachokumbuka ni Ndege niliyopewa na mama yangu.”
Niliongea kwa madaha , walicheka kidogo kisha kikao chetu kiliendelea.
“na pia mizigo yote tuliyoitegemea imeingia bila matatizo.”
“kazi nzuri sana.”
Niliwapongeza , na huo ndio ulikuwa utamaduni wangu tangu nilipoingia rasmi katika ofisi hiyo ambayo mama yangu aliianzisha miezi mitatu baada ya kuzaliwa kwangu , huwezi kuamini nikikuambia hili, nilianza kutia sahihi za ofisi hiyo hata kabla sijaanza kulitaja jina langu , dole gumba langu lilikuwa likitumika kuingiza mamilioni wakati mimi hata pesa sijui ni kitu gani na wala kina maana gani katika maisha na nilipoingia shule masomo yote niliyokuwa nasoma yalikuwa yakiniongoza kuiongoza kampuni hiyo , na kulikuwa na somo maalumu ambalo nilikuwa nikifundishwa kujifunza kuhusu kampuni hiyo , ilipo shuka ilipopanda yote nilikuwa nikipewa taarifa , uzembe uliofanyika na bidii ambayo wafanya kazi wa kampuni hiyo wameifanya.
Nakumbuka mtu wa kwanza kufukuzwa kazi kwa amri yangu ilikuwa kipindi nikiwa darasa la sita.
Nilipewa lipoti ya mtu aliyeikosesha kampuni tenda ya mamilioni ya shilingi , kwa sababu alitapika kwenye kikao cha kushindania tenda hiyo na matapishi yake yakawa yananukia pombe. Na hivyo akaiangusha kampuni ikaonekana inaendeshwa na wafanyakazi walevi.
Kwa wakati huo mama yangu aliniambia kwamba , ‘umefanya kitu sahihi’
Na jambo hilo nilikuwa nalo kwa kweli katika ofisi yangu kila mfanya kazi alikuwa nalifahamu jambo hilo vema , tulicheka pamoja na kutaniana , lakini ilipofika suala la uzembe katika kazi , nilikuwa mtu mwingine.
“hii ni kazi, siko tayari kuona mtu analeta mzaha hapa, Mr John , utawajibika katika hili , nataka maelezo ya kutosha kuhusu fedha hizo la sivyo utazilipa au utaozea jela.”
Hivyo ndivyo nilivyokuwa sikuwa tayari kuona kampuni hii ikiteteleka hata kidogo sababu ya uzembe wa mtu mmoja.
Sababu niliamini kwamba kampuni hii imeshikilia maisha ya watu wengi, nilikuwa na vituo viwili vya watoto yatima waliokuwa wakipewa matunzo yote pamoja na elimu kwa kutegemea kampuni hii , sikutaka kuwaaangusha watoto hawa na wala sikutaka kuiaibisha familia yangu kwa kunifunza jinsi ya kuendesha kampuni tangu nilipokuwa mdogo alafu leo hii kampuni iishie kufirisika,  hapana hilo kamwe sikuwa tayari kulishuhudia likitokea katika maisha yangu.
Baada ya kikao nilimuita mwana sheria wangu kwa sababu nilitaka kurekebisha mambo fulani katika kampuni.
Nikiwa nimeketi na mwanasheria huyo  ghafla simu yangu ya mkononi iliita nilipoiangalia kioo nikaiona picha ya mke wangu ,  nilitabasamu na kisha kuipokea.
“honey njoo nyumbani , ninaumwa , njoo haraka please nakufa!”
Mke wangu aliongea kwenye simu huku akilia na kisha akakata simu.
“hallo!  Halo! Halo!”
Niliita japo kuwa simu ilikuwa imekatika , nilijaribu kuipiga tena lakini haikupokelewa.
Kusema kweli jambo hilo lilinishtua kupita kiasi, nilishtuka huku akili yangu ikiwa kama vile imepagawa sikujua nifanye nini au nilekee wapi , kuisikia sauti ya mke wangu ikisikika kama ambavyo ilisikika muda huo kwenye simu ilikuwa ni mara yangu ya kwanza .
Nilianza kuhofia kumpoteza siku hiyo.
“hatuwezi kufanya hili , nimepata dharula .”
Nilimwambia mwanasheria huku nikitoka ofisini haraka.
“lakini bosi….”
Alitaka kuongea lakini alijua kwamba ameshachelewa kwa wakati huo nisingeweza kumsikiliza mtu yoyote akisema jambo lolote , hata sekritali sikumuaga nilitoka mbio huku nikiwa sijielewi kabisa , kichwani mwangu kulikuwa na picha ya mke wangu akilia na kulalamika , sikujua ni nini kina muumiza , lakini nilijua ya kwamba natakiwa kuwa pale nikimsaidia kwa lolote.
Sikuwa tayari kumruhusu afe kwa urahisi namna hii wakati bado namuhitaji.
bado nilitaka kufurahi pamoja na yeye
Niliingia kwenye gari haraka , na dereva alifanya hivyo , kisha nikamuamrisha.
“endesha gari kwa kasi nataka kufika nyumbani sasa hivi mke wangu anatatizo.”
“sawa bosi .”
Aliitikia na kisha kuzipangua gia za gari hilo , na kweli kasi yake ilikuwa balaa , japo kwangu niliona bado kabisa , nilitaka kufika nyumbani kama vile muujiza  ili nimuone mke wangu dakika hiyo hiyo.
***                                              
Nusu saa baadae tuliwasili katika makazi yangu, mimi nilishuka hata kabla gari haijasimama vizuri na kuanza kukimbia kuelekea ndani haraka.
“judy ! , Juddy ! , uko wapi malaika wangu?”
Nilianza kuita huku nikipanda ngazi za kulekea chumbani kwetu haraka .
Nilipofika chumbani nikamkuta amelala kifudi fudi huku akiwa amejikunja kwenye kona ya kitanda .
Kwa kumuangalia tu nilijua kwamba mke wangu yupo katika maumivu makali , japo sikujua kinachomuuma.
“mke wangu , umepatwa na nini malaika wangu?”
Niliongea kwa sauti ya upole  huku nikitembea haraka kusogea pala kitandani na nilipofika nilipanda hata bila ya kuvua viatu.
Nilimshika mabega na kujaribu kumgeuzi ili niweze kuiona sura yake , nilijua ya kwamba itakuwa imejaa machozi na huzuni tele lakini nilitaka kuiona hivyo hivyo hata kama matokeo ya kuiangalia yatakuwa ni  kuniliza na mimi pia.
Nilitaka kuiona ili nimuulize kile kilichomsibu wakati nayaangalia macho yake .
“tafadhari mke wangu naomba unitazame.”
Niliongea kwa sauti ya upole na yenye kubembeleza machozi tayari yalikuwa yameshaanza kuyalenga macho yangu na kile nilichokitarajia sekunde chache zijazo ilikuwa ni macho hayo kuanza kudondosha machozi.
Nilimgeuza na pale alipogeuka nilijikuta nashangaa , macho yangu yalidondosha matone ya machozi yaliyodondoka toka kwenye jicho langu na kwenda kutua moja kwa moja kwenye mashavu yake , lakini hajabu chozi hilo lililodondoka toka kwenye macho yangu ndio lilikuwa chozi pekee lililoyagusa mashavu yake kwa wakati huo.
Macho yake yalikuwa makavu na wala hayakuwa na dalili za kuwa yalitoa machozi hata dakika kadhaa zilizopita.
Macho yetu yaligongana kwa sekunde kadhaa huku mimi bado nikishangaa, na kilichofuata baada ya hapo toka kwa Juddy kilikuwa ni kicheko, alikuwa akinicheka mimi, alinicheka kwa kuwa alifanikiwa kunifanya mjinga asubuhi hiyo.
Kusema kweli nilipenda utani lakini huu alioufanya  mke wangu leo hata sikuufurahia , nilifanya kila kitu kwa haraka nikiwa ofisini nilimshinikiza dereva kwenda mwendo kasi usiokuwa wa kawaida jambo ambalo lingeweza hata kunifanya nipate ajali na mbali na yote roho yangu ilikuwa juu juu wakati wote  nikimuhofia lakini matokeo ya yote hayo ni huu utani wake.
“kwa nini umeamua kunistua hivi malaika wangu jamani?”
Nilimuuliza kwa upole , japo moyoni nilitamani hata kufoka.
Lakini jibu nililo lipata toka kwake ni kuchekwa alinicheka kicheko cha sauti ya juu na kunifanya nizidi kukasirika , lakini kwake ilikuwa marufuku kumuonyesha hasira zangu, hata niwe nimepita kikomo cha hasira nilitakiwa kuigiza ili nihakikishe anabaki katika hali ile ile ya kuwa na furaha, najua unaweza kusema mimi nina wazimu , najua kuna wakati katika maisha yangu niligundua kwamba hata nijighulishe kwa kiasi gani kamwe sitoweza kuifanya nafsi yangu ikafurahi kwa asilimia zote , lakini kitu nachoweza kufanya ni kumfanya mtu anifurahie mimi wakati wote na nilimchagua yeye , ni yeye ndiye mtu pekee ambaye kwa gharama yoyote nitahakikisha anafurahia kuwa na mimi katika maisha yake yote.
“usifanye mzaha mke wangu , namna hii unaweza kuniua.”
Nilizidi kumbembeleza japokuwa kwake bado kilikwa kichekesho alitaka kucheka zaidi ya hapo .
“nimekupata leo.”
 Aliongea na kuendelea kucheka , hapo sasa sikuwa na jinsi ili niweze kuendana nae ilinibidi na mimi nicheke pia , nilicheka utafikiri kweli nillifurahishwa na hali hiyo .
“jamani mpenzi wangu usinikasirikie , nilikumisi ndio maana niliamua kufanya hivyo.”
Aliongea mke wangu huku akiniangalia usoni, kusema kweli pamoja nakuificha hasira yangu kiasi hicho lakini juddy alikuwa na kipaji cha kuifichua hasira yangu popote pale ilipo.
Maneno yake na sauti yake vyote vilikuwa na nguvu iliyokuwa inaweza kuifutilia mbali hasira hiyo ndani ya moyo wangu.
“sawa mke wangu , siku nyingine naomba usifanye hivyo , unaweza kuwa na tatizo kweli harafu mimi nikapuuzia na kufikiri ni moja kati ya huo utani wako.”
Niliongea kwa upole.
“basi mpenzi wangu nisamehe , sirudii tena kufanya hivi nakuahidi.”
 Aliongea kwa sauti nyororo sauti ambayo ilinifanya nitulie kimya na kuyaangalia macho yake kwa hisia , sura yake na uzuri wote alionao vyote vilinifanya nipagawe kwa wakati huo , hakukuwa na huzuni wala masononeko katika moyo wangu tena bali penzi zito lililojaa uchu. Nilichokuwa natamani kwa wakati huo ni kuibusu midomo yake , kuishika sura yake nihisi ulaini wa ngozi yake .
MWISHO WA KITABU CHA KWANZA.
 AHSANTE KWA KUFUATILIA SIMULIZI ZANGU,


No comments:

Post a Comment